Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Siku chache baada ya kutangazwa kwa matokeo ya mtihani wa KCSE wa mwaka wa 2015, viongozi wa kaskazini mashariki wamejitokeza na kutaka serikali kuu kufanya usawa katika sekta ya elimu nchini.

Wakizungumza siku ya Jumapili kwenye mkahawa mmoja eneo la Riverside, jijini Nairobi, Gavana wa Wajir Ahmed Abdullahi, na mwenzake wa Garissa Nathif Jama, waliitaka serikali ya kitaifa kuhakikisha kuwa wanapeleka walimu wa kutosha katika eneo hilo ili wanafunzi wa maeneo hayo kupata matokeo mema katika mitihani ya kitaifa.

“Matokeo duni tuliyoona kwenye mitihani ya kitaifa yamesababishwa na uhaba wa walimu katika mkoa huu wetu wa kaskazini mashariki, “ alisema Gavana Abdullahi.

Vile vile, gavana huyo alisema kuwa walimu wengi waliacha kufunza shule za mkoa huo wakihofia maisha yao baada ya wenzao kushambuliwa na wanamgambo wa al-Shabaab mwaka uliopita.

“Idadi kubwa ya walimu waligura maeneo yetu wakati visa vingi vya utovu wa usalama vilishuhudiwa. Nafasi walizoacha hazikujazwa, hali ambayo imeathiri viwango vya masomo na kuchangia matokeo yasiyoridhisha kwenye mitiihani ya kitaifa,” alisema Abdullahi.

Gavana wa Garissa kwa upande wake alisema kuwa kufuatia matokeo duni waliyoyapata wanafunzi wa mkoa huu, huenda wengi wao wakajiunga na makundi ya kigaidi.

“Wanafunzi ambao wamepata alama yasiyoridhisha huenda wakajiunga na makundi ya kigaidi kwa kuwa hawana la kufanya maishani,” alisema Gavana Jama.

Magavana hao walikuwa wameandamana na Seneta wa Kaunti ya Garissa Yussuf Haji na wabunge kadhaa kutoka eneo hilo.