Serikali imetakiwa kuunda kitengo maalum cha kukabiliana na visa vya udanganyifu wa mitihani ya kitaifa nchini.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumamosi, kiongozi wa vijana katika eneo la Kisauni mjini Mombasa, Maxwell Masai amesema kwamba kushuhudiwa visa vya udanganyifu wa mitihani kunadidimiza viwango vya elimu pamoja na kudhalilisha sekta hiyo kote nchini.
Masai imeitaka wizara ya elimu nchini na baraza la mitihani nchini KNEC kuidhinisha sheria kali zitakazozuia kuenea kwa udanganyifu wa mitihani ya kitaifa.
“Tungependa kuona serikali ikibuni kitengo maalum cha kuzuia kuenea kwa visa vya udanganyifu wa mitihani ya kitaifa kwa sababu hali hii ni aibu kwa taifa letu na inadhalilisha sekta ya elimu,” alisema Masai.
Hatua hii ni baada ya kushuhudiwa visa vingi vya udanginyifu kwa kupatikana makaratasi ya mitihani inayodaiwa kuwa sawia na ile inayoendelea kwa sasa kusambazwa kwa wanafunzi.
Hata hivyo, baraza la mitihani nchini KNEC kwa ushirikiano na maafisa wa upelelezi limefanikiwa kutambua mtandao unaoamika kutumika kusambaza karatasi za mitihani ya udanganyifu.
Baraza hilo limetangaza baadhi ya mikakati itakayotumika kukabili wizi wa mitihani nchini, huku likitoa onyo kali kwa wale watakaopatikana wakiendelea kuwalaghai wanafunzi kuwa watakabilina na sheria.