Serikali imetakiwa kubuni mbinu mbadala zitakazohakikisha kuwa watoto wanaoranda randa mitaani hasa katikati ya mji wa Mombasa wahifadhi vyema ili kupata msingi bora wa kimasomo na kuwasaidia katika siku za usoni.
Mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Mombasa Mishi Mboko amesema kuwa familia zinazoomba barabarani hasa katikati mwa mji zimeongezeka na kusababisha watoto wengi kusambaa mjini humo, kuomba pesa na vyakula kwa watu wasio wafahamu na hali hiyo ni hatari kwa jamii.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Mboko alisema kuwa lazima serikali kuu na ile ya Kaunti ya Mombasa kuibuka na sheria dhabiti zitakazowasadia watoto hao hususana wale wa kike ili kuepukana na kukithiri kwa dhulma za kijinsia na uhalifu.
"Tunaitaka serikali kuu na ile ya Kaunti ya Mombasa kuibuka na mikakati mwafaka ya kuhakikisha kuwa watoto wa kurandaranda mjini wanachukuliwa na kuhifadhiwa ili kuona kuwa wanapata msingi bora wa maisha na masomo na kuwasaidia katika siku za usoni," alisema Mboko.
Mboko amesisitiza kuwa iwapo swala hilo litachukuliwa kwa uzito, basi watoto hao watasaidika kimasomo, kiafya na kuwa katika mazingira bora ili kuinua kizazi kijacho kuepukana na kusajiliwa na makundi ya kihalifu na ugaidi pamoja na kuepukana na visa vya ubakaji.