Share news tips with us here at Hivisasa

Rais Uhuru Kenyatta ametakiwa kutimiza ahadi yake ya kupendekeza taasisi ya huduma ya vijana kwa taifa NYS eneo la Miritini itumiwe kama kituo cha kuwarekebishia tabia watumizi wa mihadarati.

Mbunge wa Jomvu Badi Twalib alisema kwamba wasimamizi wa taasisi hiyo hawajakumbatia pendekezo hilo na kusababisha changamoto nyingi katika kuwanasua waathiriwa wa dawa za kulevya licha ya Rais Uhuru kutoa kauli hiyo.

Akizungumza katika kituo cha kurekebisha waathiriwa wa mihadarati cha ‘Reach out’ eneo la Mtongwe mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Badi alisema kwamba iwapo taasisi hiyo ya NYS itatekeleza jukumu hilo basi itapunguza idadi kubwa ya waathiri wa mihadarati.

“Tunamtaka Rais Kenyatta kutimiza ahidi aliyotoa kwa wakazi wa Mombasa kuhusu kutenga eneo la NYS pale Miritini na kutumika kama kituo cha kurekebisha tabia waathiriwa wa mihadarati”,alisema Badi.

Badi alisema kwamba atahakikisha kwamba wanaonasuliwa kutokana na jinamizi hilo wanasaidika na miradi mbalimbali ili kujikimu kimaisha.

Jumla ya iijana saba kutoka eneo bunge la Jomvu wanapokea ushauri na tiba katika kituo cha 'Reach' out huko Mtongwe huku mbunge huyo akisema kwamba baada ya muda wa miezi mitatu watumizi wengine saba vile vile watasajiliwa katika kituo hicho.