Share news tips with us here at Hivisasa

Ni lazima kwa kitengo maalum cha kupambana na ugaidi nchini Recce Squad kutengewa makao katika kila kaunti ili kukabiliana vilivyo na ugaidi.

Kulingana na Seneta Maalum wa Kaunti ya Mombasa Emma Mbura, tukio la hivi majuzi la shambulizi katika mjini wa Paris nchini Ufaransa ni la kusikitisha mno na kuna haja ya kitengo hicho maalum kuidhinishwa katika kila kaunti.

Akiongea mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Bi Mbura alisema ni lazima kwa serikali kupitia Wizara ya Usalama wa Ndani na ile ya ulinzi nchini kufanya vikao vya majadiliano na kuafikiana kwa kauli moja ili kitengo hicho cha Recce Squad kutengewa makao yake katika kila kaunti ili kuwalinda vyema wananchi.

“Wakenya tumekuwa tukishambuliwa na makundi ya kigaidi na sasa tumeona taifa lililo na uwezo zaidi la Ufaransa pia likishambuliwa, basi sisi kama viongozi tunaiomba serikali kutuma kitengo maalum cha Recce Squad katika kila kaunti ili kuwalinda wakenya," alisema Bi Mbura.

Kauli ya Seneta huyo Maalum inajiri huku serikali ikifanya kila juhudi kuimarisha usalama kote nchini kwa kutuma vitengo vya wanajeshi mashinani.