Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali ya kitaifa imetakiwa kujibidiisha kutoa fedha za kufadhili elimu ya bure katika shule za msingi za umma.

Akizungumza kwenye mahojiano na mwandishi huyu mjini Nakuru siku ya Jumatatu, mwalimu mkuu wa Shule ya msingi ya Nakuru West iliyoko viungani mwa mji wa Nakuru, Francis Macharia, alisema kuwa ucheleweshaji wa fedha hizo kwa wakati mwingi hutatiza mipango ya shule.

“Ufadhili unaotolewa na serikali kupitia kwa wizara ya fedha ya kufanikisha elimu ya bure huwa unachelewa. Tulifungua shue tarehe nne mwezi Januari na fedha za serikali zilifika mwisho wa Februari. Hatua hiyo huwa inatatiza shughuli mbalimbali zilizopangwa shuleni,” alisema Macharia.

Hata hivyo, mwalimu huyo alisema ili kufanikisha mipango hiyo kwa wakati ufaao, fedha hutafutwa kwingineko na kisha kurejeshwa baada ya fedha za kufadhili elimu ya bure kutolewa na serikali kwa shule hizo.

“Huwa tunapanga pamoja na bodi ya shule na kisha tunakubaliana kukopa fedha hizo kwingineko na kisha kuzirejesha serikali inapotoa fedha hizo,” alisema Macharia.

Haya yanajiri huku serikali ikiwa na nia ya kutoa elimu ya sekondari bila malipo kwa muda wa miaka mitano ijayo.