Mwenyekiti wa shirika la kijamii la watu wanoishi na ulemavu katika maeneo ya Changamwe, Kaunti ya Mombasa James Karanja, ameitaka serikali kuharakisha mswada wa ujenzi wa kuboresha majengo yote nchini, ili kurahisisha matembezi ya walemavu katika maeneo mbali mbali nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya kupeana viti magurudumu katika eneo la Changamwe, Karanja alisema kuwa iwapo mswada huo utapitishwa, watu wanaoishi na walemavu wataweza kujihusisha katika miradi mbali mbali na kuendeleza maisha yao vizuri.
Aidha, Karanja ametoa wito kwa watu wanoaishi na ulemavu kujiunga katika makundi ili kuwawezesha kunufaika na miradi kupitia mipangilio ya ugatuzi na kuwawezesha kutoa changamoto zao kwa umoja.
Vilevile, msimamizi wa shirika la kitaifa la walemavu nchini Sarah Ayecho amewataka wazazi kutowaficha watoto wanaoishi na ulemavu ili mipangilio yao iweze kubainika na kuwekwa sawa.
Kulingana na Ayecho, watoto wanaoishi na ulemavu wakifichwa hukosa huduma kulingana na mipangilio ya serikali.
Shirika la kitaifa la walemavu nchini lilipeana viti magurudumu 100 katika Kaunti ya Mombasa huku watu wanaoishi katika eneo la Changamwe wakipata viti 20 na mikongojo 10.