Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuzindua mradi wa kitaifa wa kuweka mataa barabarani katikati ya miji mikuu nchini ikiwemo mji wa Mombasa ambapo zaidi ya shilingi milioni 224 zimetengewa mradi huu.
Esipisu msemaji wa Ikulu ya Rais siku ya Alhamisi mjini Mombasa, alisema kuwa mradi huo unaofahamaika kama Mwangaza Mtaani ukiwa ni sehemu ya mradi unaofahamika kama Uhuru wa Umeme, utasaidia kuimarisha ustawi wa viwanda na ukuzaji uchumi na pia utawezesha kuendeleza shughuli za kiuchumi kwa saa 24.
"Serikali imetenga shilingi milioni 224 kutumika kwa mpango wa kuweka mataa katika barabara za mji mjini Mombasa, shilingi milioni 62 kaunti ya Kwale na shilingi milioni 94 kuanti ya Kilifi ili kuhakikisha kuwa masuala ya uchumi yanatekeleza saa 24," alisema Esipisu msemaji wa Ikulu ya Rais.
Kupitia mradi huo serikali inatarajiwa kuwanufaisha Wakenya kwa kuongeza nafasi za kazi, kuongeza uzalishaji wa kawi na teknolojia ili kuhakikisha kuwa masuala ya kiusalama pia yaangaziwa.
Maeneo ambayo yatafaidika na mradi huo katika kaunti ya Mombasa ni maeneo ya Nyali, Changamwe, Mji wa Kale, Likoni, Majengo, Bondeni na Kongowea huku kaunti ya Kwale ikiwemo maeneo ya barabara ya Diani, Kwale, Ukunda na Tiwi kwa gharama ya shilingi milioni 62.
Maeneo ambayo yametengewa mradi huo katika kaunti ya Kilifi ni barabara ya Malindi, Watamu, Timboni na Gede kwa gharama ya shilingi milioni 94 ili kuhakikisha kuwa maswala ya kibiashara, utalii na usalama yanaekezwa zaidi.
Mpango huo wa kitaifa wa kuweka mataa barabarani kwa sasa unatekelezwa katika mji mkuu ya Nairobi, Kisumu, Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet, Nyeri, Kiambu na Pokot Magharibi katika juhudi za kuendeleza shughuli za kiuchumi kwa saa 24.