Serikali imetenga kima cha shilingi milioni 300 kutumika katika upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Malindi ili kuimarisha sekta ya uchukuzi na utalii.
Akizungumza katika chuo kikuu cha Pwani kaunti ya Kilifi siku ya Jumamosi, Naibu Rais William Ruto alisema kuwa shughuli za kufidia wananchi wanaoishi karibu na uwanja huo zitaanza rasmi.
Ruto alisema kuwa sekta ya utalii humu nchini imeanza kuimarika na upanuzi wa kiwanja hicho cha ndege kuisaidia pakubwa kukuwa kwa sekta hiyo iliyokumbwa na cahangamoto.
“Kama serikali tumetenga kima cha shilingi milioni 300 zitakazotumika katika kupanua kiwanja cha ndege cha Malindi ili kuhakikisha kuwa tunaboresha sekta ya utalii na uchukuzi katika kaunti hii,” alisema Naibu Rais.
Aidha, amewataka maafisa wa polisi eneo la Pwani kuzidi kuimarisha usalama na kuwawezesha wadau katika sekta hiyo kuekeza zaidi.
“Na maafisa wetu wa usalama, tafadhilini fanyeni kazi nzuri ya kuhakikisha usalama unaimarisha na kuwalinda wananchi wetu ili kuhakikisha maswala ya uwekezaji na uchumi wa nchi unaimarika,” alieleza Ruto.