Huku misongamano ya magari ikiendelea kushuhudiwa katika barabara zote zinazoingia mjini Kisii, serikali imeombwa kupanua barabara hizo ili kupunguza misongamano hiyo.
Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu mjini Kisii, wakazi, wahudumu wa matatu na wale wa bodaboda wakiongozwa na Dismus Omariba waliomba serikali kupanua barabara zote za kuingia katika mji wa Kisii ili kupunguza misongamano ya magari na piki piki.
Kulingana nao, misongamano hushuhudiwa kila wakati kupitia ukosefu wa upanuzi wa barabara hizo ambazo walisema ziko nyembamba zaidi na kuna haja ya kupanuliwa.
“Tunaomba serikali kujaribu kila iwezalo kuhakikisha misongamanao katika barabara zote zinazoingia katika mji wa Kisii zinapanuliwa ili kupunguza misongamano,” alisema Omariba.
Baadhi ya barabara ambazo walitaka zirekebishwe miongoni mwao ni barabara ya kutoka Daraja Mbili kuelekea mjini Kisii, Mwembe kuelekea mji huo, Denmark kuingia mjini Kisii pamoja na ile ya Laumu –Kisii.
Wakati huo huo, serikali pia iliombwa kuweka matuta katika barabara hizo za kuingia mjini Kisii ili kupunguza ajali ambazo hufanyika kila mara kupitia uendeshaji mbaya wa madereva.
“Wakati serikali itafanya upanuzi au kabla ya kupanua barabara hizi, tunaomba matuta yawekwe katika barabara hizi zote za kuingia mjini Kisii ili visa vya ajali viweze kuzuiwa,” alisema Martha Kerubo, mkazi.