Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wafanyibishara wa soko la Keroka wamezikosoa serikali za kaunti ya Nyamira na kaunti ya Kisii kwa kutumia vyombo vya habari kuwa serikali hizo zimefanya maendeleo katika soko hilo ilhali hakuna maendeleo yaliyofanywa.

Kulingana na wafanyibiashara hao, serikali ya kaunti ya Kisii ilisikika ikisema kupitia vyombo vya habari kuwa ilitumia shillingi million 1.9 kutengeneza vyoo vya soko la Keroka huku serikali ya kaunti ya Nyamira ikisema kuwa ilitumia shillingi millioni 16 kukarabati barabara na soko hilo, mambo ambayo wafanyibiashara hao wamekana.

Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano katika soko hilo, wafanyibiashara hao, wakiongozwa na Christopher Maina na Keneddy Ombui walisema serikali hizo hazijafanya maendeleo katika soko hilo.

Mnamo siku ya Jumanne wiki hii, wafanyibiashara wa soko hilo waliandamana kulalamikia kutofanyiwa maendeleo, na kuomba gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae na wa Nyamira John Nyagarama kujiunga pamoja na kuwaeleza soko hilo liko katika kaunti ipi ili wafanyiwe maendeleo.

Soko la Keroka liko katika mpaka wa kaunti ya Kisii na ya Nyamira, huku wakisema hakuna vyoo vya soko, mazingira mabaya, kutokarabatiwa kwa soko miongoni mwa mengine.

“Tunaomba serikali hizi mbili ziwache kudanganya watu kuwa wamefanya maendeleo katika soko letu la Keroka, tunahitaji ukweli na haki yetu kwani tuliwachagua kufanya maendeleo bali si kudanganya wananchi,” alisema Maina.

Mwakilishi wa wadi ya Ichuni Francis Aburi aliunga mkono matamshi ya wafanyibiashara hao, huku akiomba serikali hizo kufanya maendeleo katika soko hilo