Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali za kaunti eneo la Pwani zimetakiwa kufanya utafiti na kubaini idadi kamili ya watu wanaoishi na ulemavu ili kuyawezesha mashirika yasiyo kuwa ya kiserikali kutambua jinsi yatakavyoisadia jamii hiyo.

Akizungumza katika karakana ya walemavu ya Bombolulu mjini Mombasa siku ya Jumapili, Daktari Samson Makanga wa Shirika la APDK alisema kwamba imekuwa changamoto kwa mashirika hayo kutafuta ufadhili kufuatia ukosefu huo wa takwimu.

Makanga amesema kuwa ni lazima serikali za kaunti eneo la Pwani kuwa na takwimu hizo na iwapo zitahitajika, kaunti hizo ziwe tayari kuzitoa kwa minajili ya kupata ufadhili.

“Tunaziomba serikali za kaunti eneo la Pwani kubaini takwimu ya watu wanaoishi na ulemavu ili kuyawezesha mashirika ya kijamii kusaidia jamii hiyo,” alisema Makanga.

Mtaalam huyo wa afya ya walemavu amehimiza ushirikiano kati ya mashirika yanayopigania haki za walemavu, serikali za kaunti na serikali kuu ili kuisaidia jamii hiyo na wala sio malengo ya kibinafsi.

“Tunawataka viongozi wa serikali za kaunti hapa Pwani, serikali kuu na mashirika ya kutetea maslahi ya walemavu kushirikiana vyema na kusaidia jamii ya walemavu kuepukana na changamoto wanazopitia,” aliongeza Makanga.