Gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae ameomba serikali zote za kaunti nchini kushirikiana na serikali ya kitaifa kupambana na ugaidi kuleta usalama.
Ongwae alitangaza kuwa serikali yake itashirikiana na serikali ya kitaifa kupambana na ugaidi kuhakikisha kuna usalama wa kutosha kwa wananchi.
Akizungumza siku ya Jumapili katika uga wa Gusii stadium, Ongwae alisema kuna haja ya serikali za kaunti zote nchini kushirikiana na serikali kuu kuleta usalama kwa kupambana na ugaidi huku akisema tayari serikali yake ya kaunti ya kisii imejitolea kufanya hivyo.
Ongwae alikemea mashambulizi yaliyoshuhudiwa nchini Somalia ambapo baadhi ya wanacheshi wa KDF waliuawa na kusema serikali ya Kenya itaendelea kupambana na kundi la Al Shabaab nchini humo hadi usalama ushuhudiwe.
“Naomba serikali zote za kaunti tujiunge pamoja na tushirikiana na serikali ya kitaifa kuhakikisha kuna usalama wa kutosha nchini na ata kwa nchi jirani,” Ongwae alisema.
Ongwae aliomba kila kijana kutafuta njia ya kujipatia pesa wala si kujihusisha na vikundi ambavyo sio halali ili kupata pesa huku akisema maisha ya wale wanaojiunga na vikundi hivyo huwa mafupi mno.
“Naomba kila kijana kutafuta mbinu ya kupata pesa kwa kila siku na musijihusishe na vikundi vya mashambulizi kama al shabaab kwani vikundi hivyo sio halali,”aliongeza Ongwae.