Mwakilishi wa walemavu katika kaunti ya Mombasa Herdson Karume ametoa wito kwa serikali za kaunti kutowakamata na kuwasumbua walemavu wanaoomba omba katikati ya jiji.
Akizungumza na wanahabari siku ya Jumatatu katika makao ya bunge la Mombasa, Karume alizitaka serikali za kaunti kuwapa ajira walemavu ambao wako na visomo vya taaluma mbali mbali.
"Kuna walemavu wengi ambao wako na elimu na ujuzi wa hali ya juu, naomba waweze kusaidiwa katika kutafuta ajira ili wajikimu kimaisha," alisema Karume.
Karume aliyasema haya baada ya kupokea msaada wa viti vya watoto walemavu, hivyo kuwapa changamoto viongozi katika kaunti nyengine kwamba ziweze kufanya kama kaunti ya Mombasa ilivyofanya.
Aidha, aliwasihi wahisani wa kibinafsi kujitokeza ili kusaidia walemavu katika kila kaunti.
Viti hivyo vitagawanywa viwili viwili kwa kila shule iliyo na watoto walio na ulemavu wa kutembea.