Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwenyekiti wa tume ya usawa wa jinsia NGEC, Winfred Lichuma, amesema serikali za kuanti zinapaswa kuwatambua waliotengwa kuambatana na katiba mpya ya Kenya.

Akizungumza baada ya kumtembelea Gavana wa Nakuru Kinuthia Mbugua afisini mwake siku ya Ijumaa, Lichuma alisema kuwa tume hiyo imejitolea kuhakikisha kwamba lengo lake kuu la kumaliza dhuluma za kijinsia katika kaunti zote za Kenya limeafikiwa.

“Hapo awali, swala la waliotengwa lilipozungumziwa, wengi walifikiria kuhusu jamii iliyo katika eneo la Kaskazini Mashariki, lakini tukiangalia katika kaunti, tunatarajia kila kaunti itaangalia wakazi wake ili kuweza kubaini kundi la watu linalofaa kuwa kati ya wanaotajwa kama walio wachache na waliotengwa,” alisema Lichuma.

Aliongeza, “Sisi kama tume tunataka kubaini iwapo hilo ni jambo ambalo kaunti ya Nakuru imefanya au inafanya na kwa kufanya hivyo, kaunti inaweza kujua njia za kujiendeleza na mahala pa kurekebisha.”

Lichuma alisema kwamba kampeni hiyo imetokana na sheria zilizobora za kukabiliana na dhulma za kijinsia kama ile ya kukabiliana na ukeketaji miongoni mwa sheria zingine.

Mwenyekiti huyo alisema tume ya NGEC iko tayari kufanya kazi kwa pamoja na serikali za kaunti ili kubuni miswada ya kukabiliana na dhulma za kijinsia katika viwango vya kaunti.

“Kama tume, tungependa kujua iwapo serikali za kaunti zina miswada ya kukabiliana na dhulma za kijinsia ambazo tunaweza kusaidia katika harakati za kuifanya kuwa sheria, au kama kuna miswada ambayo tunaweza kusaidia katika uandishi wake, ili kuwa sheria ya kaunti inayolenga kukabiliana na dhulma za kijinsia,” aliongeza Lichuma.

Kwa upande wake, Gavana Mbugua alipongeza tume hiyo kwa kazi yake nzuri, kwa kusema kuwa tume hiyo ni mojawapo ya matunda yanayotokana na katiba mpya ya Kenya.

“Hatua ya katiba ya Kenya kutengea nafasi tume hii inaonesha kujitolea kwa Kenya katika kuangazia na kukabiliana na swala la dhulma za kijinsia,” alisema Mbugua.