Share news tips with us here at Hivisasa

Mazungumzo baina ya serikali ya kitaifa na kaunti ya Kilifi yameanza rasmi kujadili jinsi ya kufufua kiwanda cha korosho mjini Kilifi.

Kiwanda hicho kinatarajiwa kusaga korosho utakaovuniwa kwenye kaunti za Kilifi, Mombasa na Kwale.

Waziri wa Kilimo, Ufugaji na Ustawi wa Uvuvi katika kaunti ya Kilifi Mwalimu Katana Menza alisema serikali ya kaunti hiyo tayari imetenga kima cha shilingi milioni 20 katika bajeti ya mwaka huu kufufua kiwanda hicho kilichosambaratika.

Akizungumza katika kongamano la kibiashara lililoandaliwa mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Menza alisema juhudu hizo zitasaidia pakubwa kuimarisha uchumi wa jamii ya wapwani sambamba na kubuni ajira kwa vijana.

Menza aliwaomba wabunge wa kitaifa kuunga mkono mpango huo ili kuhakikisha kwamba wakazi wa kaunti ya Kilifu na eneo zima la pwani wananufaika na kiwanda hicho.

“Kama serikali ya kaunti ya Kilifi tumetenga kima cha shilingi milioni 20 kutumika kufufua kiwanda cha korosho kilisambaratika na tunawaomba wabunge wa kitaifa kuunga mkono mpango huo ili serikali kuu itusaidie na fedha zaidi kufanikisha mradi huo," alisema Meza.

Kiwanda hicho kilisambaratika kutokana na madai ya uongozi mbaya na kukithiri kwa kashfa za ufisadi kutoka kwa baadhi vya viongozi wa serikali na kutokana na hilo kukapelekea kuuzwa kwa mwekezaji mmoja.