Shirika la huduma za feri katika kivuko cha Likoni limepewa makataa ya siku 10 kufanya mabadiliko kuboresha huduma katika kivukio hicho, ama wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wafanye maandamano.
Wakitoa makata hayo siku ya Jumatano, wanaharakati hao pamoja na baadhi ya wanasiasa wa zamani wakiongozwa na aliyekuwa mwakilishi wadi ya Bofu Ahmed Salama walilitaka shirika hilo kuboresha kivukio hicho kama njia moja wapo ya kupunguza msongamano wa abiria na magari.
Aidha, waliongeza kuwa licha ya bunge la kaunti kupitisha kurudishwa kwa feri ya Mtongwe, jambo litalopelekea upungufu wa msongamano katika kivukio hicho na kufufua hali ya uchumi wa eneo hilo, wanaulaumu usimamizi wa shirika hilo kwa kutowajibika katika suala hilo.
Vilevile wamesisitiza kuwa tatizo hilo linafaa kutatuliwa kwa haraka ikizingatiwa shule ziko karibu kufunguliwa ili shughuli za masomo kwa wanafunzi zisitatizwe.
Mara kwa mara visa vya msongamano watu na feri kukwama vimekuwa vikiripotiwa katika kivukio hicho, jambo ambalo linapotezea mda wa watumizi wa kivukio hicho na kuathiria uchumi wa nchi.
Itakumbukwa kuwa waziri wa utalii Najib Balala alisema kuwa atafanya kila awezalo kwa kushirikiana bega kwa bega na wahusika kwenye sekta ya kitalii kuimarisha hali ya utalii kwenye eneo la Pwani kama njia mojawapo ya kuwapa moyo wakazi wa maeneo hayo ambao kwa kina wanategea upataji wa riziki kutokana na shughuli za kitalii.