Share news tips with us here at Hivisasa

Shirika la utetezi wa haki za kibinadamu la Haki Afrika nchini limeshutumu vikali jinsi wakaazi wa eneo bunge la Malindi walivyomdhalilisha Mwakilishi wa bunge la kaunti ya Kirinyaga kwa madai ya kuwahonga wakaazi katika uchaguzi mdogo wa Malindi.

Afisa wa Maswala ya watoto na jinsia katika shirika hilo Salma Hemed amesema kuwa hatua hiyo ni kinyume kabisa na sheria ya nchi na waliyohusika wanafaa kuchukulia hatua za kisheria.

Akizungumza mjini Mombasa katika afisi za shirika hilo baada ya kukusanya ripoti ya ukaguzi wa uchaguzi wa Malindi, Bi Salma amesema kuwa wamebaini kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na changamoto za mitambo ya kieletroniki iliyochangia kucheleweshwa kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi huo.

Amesema kuwa idadi ndogo ya wapiga kura katika vituo vya maeneo ya Shella na mjini Malindi ilishuhudiwa kutokana na tetesi za kuzuka kwa vurugu zinazodaiwa kuchangiwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa.

"Tunalaani kitendo ambacho vijana walimfanyia Mwakilishi wa wanawake mbunge wa kaunti ya Kirinyaga ni kitendo cha kumdhalilisha mwanamke na lazima waliohusika kuchukuliwa hatua za kisheria," alisema Hemed.

Wakati huo huo amepongeza juhudi za maafisa wa usalama jinsi walivyoshika doria kikamilifu katika eneo hilo kufanikisha uchaguzi huru na haki huku akiwapa changamoto maafisa wa usalama kuimarisha usalama pia wakati wa uchaguzi mkuu.