Share news tips with us here at Hivisasa

Utafiti uliyofanywa na Shirika la Kijamii la ‘Kenya Community Support Centre', limebaini kuwa vijana wengi katika Kaunti ya Mombasa wako katika hatari ya kujiunga na mashirika yanayohubiri itikadi kali.

Akiongea na wanahabari baada ya kongamano la kiusalama katika eneo la Kisimani mjini Mombasa siku ya Jumanne, Afisa wa mipango katika shirika hilo Hassan Kibwana, alisema kwamba hatua hiyo imetokana na vijana kutohusishwa katika miradi mbali mbali ya kimaendeleo.

Kulingana na Kibwana, Kaunti ya Mombasa ndio imeathirika zaidi eneo la Pwani kwa vijana kujiunga na makundi ya misimamo mikali pamoja na kuvuruga usalama wa kaunti hiyo, hali ambayo inahitaji kushughulikiwa kwa dharura ili kuwaepusha vijana na maswala hayo.

Kibwana aliwataka jamii kushirikiana kwa karibu na maafisa wa usalama kwa kutoa habari kuhusu washukiwa wa ugaidi na wahalifu ili kutiwa nguvuni na kuimarisha usalama katika kaunti hiyo na eneo zima la Pwani.

"Utafiti tuliofanya kama shirika tumebaini kuwa vijana wengi katika Kaunti ya Mombasa wamejiunga na makundi ya itikadi kali kutokana na kutohusishwa kikamilifu na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo," alisema Kibwana.

Hata hivyo, shirika hilo la kijamii limo mashinani kuwahamisha vijana kufahamu jinsi ya kujiepusha na vishawishi vibaya kutoka kwa makundi ya kigaidi na kihalifu na kujiunga na maswala ya misimamo mikali.

Bw Kibwana aliongea wakati Kamishna Mkuu wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa anakashifiwa na Gavana wa Mombasa Hassan Joho kwa kuwahusisha vijana kwenya kaunti hiyo na uhalifu na ugaidi.