Utafiti uliyofanywa na Shirika la Msalaba Mwekundu tawi la Mombasa umebaini kwamba mtoto wa kike eneo la Pwani angali anakabiliwa na changamoto nyingi zinazomzuia kupata elimu msingi sawa na mtoto wa kiume.
Kulingana na Christine Nzillani, afisa wa mradi unaopigania elimu kwa mtoto wa kike unaofahamika kama ‘Girl child education challenge’ na ulio chini ya Shirika la Msalaba mwekundu, mtoto wa kike ametengwa zaidi ikilinganishwa na yule wa kiume katika eneo la pwani.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Nzilani alisema kwamba changamoto ya kudhalilishwa kwa Mtoto wa kike sawa na ile ya kuozwa mapema vimekuwa vizingiti vinavyomzuia mtoto wa kike kupata elimu.
Afisa huyo aidha alisema kwamba mradi huo unaotekelezwa mjini Mombasa unalenga kuibadili hali na kuhakikisha kwamba mtoto wa kike anapata elimu ya kutosha pasipo kubaguliwa na jamii.
“Tumebaini kuwa mtoto wa kike amebaguliwa sana ikilinganishwa na mtoto wa kiume katika maswala ya elimu, na hatua hii imechangia kurudisha nyuma viwango vya elimu na kumwezesha mtoto wa kike kufanikisha malengo yake wakati wa siku za usoni,” alisema Nzilani.
Hata hivyo, afisa huyo alisema kwamba tayari shirika hilo la msalaba mwekundu linaihusisha jamii yenyewe mashinani ili kuona kwamba jamii inahamasishwa kikamilifu kuhusiana na umuhimu wa mtoto wa kike kupata elimu.