Shughuli za ujenzi zilitatizika kwa takriban masaa mawili katika eneo la Mwachamago kaunti ndogo ya Likoni kufuatia mzozo baina ya mwenye shamba na vijana almaaruf mateja.
Hii ni kutokana na madai ya kuwa hawakupewa 'pesa ya kamba', na wakatatiza shughli za mwenye shamba hilo ambay alikuwa anapima kiwanja chake ili aanze kujenga.
Akizungumza na mwandishi huyu, mwenye shamba hilo ambaye alitambulika kama Bwana Idriss, yalizuka majibizano na vijana hao, na kukashfu vitendo kama hivyo, ambavyo alisema vimeenea kwa viwango vikubwa katika eneo hilo.
"Ukionekana tu wataka kuanza mjengo utatakiwa kulipa sh3,000 au zaidi kwa mkubwa wa mateja ili uruhusiwe kuendelea na shughuli yako. La sivyo hutoruhusiwa abadan," alielezea sikitiko lake.
Matamshi yake yameungwa mkono na wakazi wengine, ambao walisema wamechoshwa na tabia hiyo na kuomba serikali ya Kaunti ya Mombasa kulishughulikia tatizo hilo la kuombwa pesa kwa upesi.