Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Shule ya upili ya Kabarak, iliyoko kaunti ya Nakuru, kwa mara nyingine ndio shule iliyosajili matokeo bora zaidi katika mtihani wa KCSE wa mwaka jana kwa mwaka wa pili mfululizo baada ya kupata jumla ya alama 11.667, ambayo ni gredi ya A.

Kati ya watahiniwa 289 katika shule hiyo walioufanya mtihani mwaka jana, 202 walipata gredi ya A, huku mtahiniwa aliyepata gredi ya chini akipata B.

Mwaka wa 2014, shule hiyo ilisajili matokeo bora zaidi nchini kwa kupata jumla ya alama 11.358 ikiwa na alama ya A, 134 A- 114, B+ 17, B 18 na B- 1.

Wengi wa wanafunzi wa shule hiyo wamefanikiwa kupata kujiunga na vyuo vikuu vya kimataifa kama vile chuo kikuu cha Ivy League nchini Marekani, huku wengi wakisajiliwa katika vyuo vikuu vya kitaifa humu nchini.

Akizungumza katika mahojiano na wanahabari Alhamisi katika shule hiyo, Bi Elisheba Cheruiyot ambaye ni Mwalimu mkuu, alisema kuwa mafanikio kwa shule yake ni kutokana na bidii ya pande zote husika, kuanzia mwanafunzi, walimu na wafanyakazi ambao hushirikiana kuhakikisha kuwa shule hiyo inapiga hatua kila wakati.

“Ningependa hasa kutoa shukrani kwa usimamizi wa shule na wazazi kwa ushirikiano mwema, pili ni wanafunzi na walimu kwa ushirikiano baina yao ambayo ndio tunasherehekea leo,” alisema Bi Cheruiyot.