Huenda shule ya upili ya Kampi ya Moto ikapata shamba la robo ekari hivi karibuni, shamba ambalo linadaiwa kunyakuliwa na bwenyenye mmoja kwenye eneo hilo.
Akizungumza kwenye kituo cha kibiashara cha Kampi ya Moto Jumatano, afisa mkuu wa tume ya ardhi nchini tawi la kaunti ya Nakuru Frank Kibelekenya alisema kuwa, kwa sasa anapitia stakabadhi ambazo ziliwasilishwa kwenye afisi yake na bwenyenye anayedaiwa kunyakua shamba hilo.
Aliongeza kuwa uchunguzi dhidi ya swala hilo uko karibu kukamilika, na ikiwa atapatikana na makosa atachukuliwa hatua kali za kisheria kwani ni hatia kunyakua mali ya umma.
“Hatuwezi kuendelea kunyamazia maswala ya unyakuzi wa ardhi haswa katika kaunti ya Nakuru. Mali ya umma ni ya umma, na mtu binafsi hana haki ya kujitwaalia mali hiyo. Uchunguzi unaendelea, na hivi karibuni tutajua ukweli,” Kibelekenya alisema.
Haya yamejiri majuma kadhaa baada ya mwenyekiti wa tume ya ardhi nchini Mohammed Swazuri kutoa amri, akimtaka bwenyenye huyo kurejeshea shule hiyo shamba lake mwishoni mwa mwaka Jana.