Serikali ina mipango ya kukarabati shule ya msingi ya Jomo Kenyatta iliyoko huko Msambweni na kuifanya kuwa yenye hadhi ya kisasa.
Akizungumza siku ya Alhamisi katika ikulu ya rais mjini Mombasa, msemaji wa rais Manoah Esipisu alisema mikakati inaandaliwa ya kuifanyia marekebisho shule hiyo, baada ya kusahaulika kwa muda ikizingatiwa shule hiyo ilipewa jina la aliyekuwa rais wa taifa hili hayati mzee Jomo Kenyatta.
Esipisu alisisitiza kuwa hatua hii itaonyesha heshima na hadhi kwa mwendazake rais wa kwanza wa taifa hili, na kuifanya kuwa kumbukumbu za mzee Jomo Kenyatta.
Msemaji huyo pia alisema hatua hii inalenga kuboresha elimu nchini, wala si jambo la kisiasa kama viongozi pinzani wanavyodai, hasa wakati serikali inajitahidi kuboresha uchumi na maendeleo ya taifa.