Walimu na wanafunzi wa Shule ya msingi ya Nyaronge wana kila sababu yakutabasamu baada yakupokea madawati kutoka kwa afisa mmoja wa Chuo Kikuu cha Kisii.
Akizungumza shuleni humo siku ya Ijumaa alipo pokeza usimamizi wa shule hiyo madawati hayo, Professa Abaya Ondigi aliipa changamoto Wizara ya Elimu kuhakikisha kuwa shule zote nchini zinapokea pesa zakutosha ili kuwezesha usimamizi wa shule husika kununua madawati yakutosha.
Ondigi alisema kuwa idadi ya wanafunzi wanaojiunga na darasa la kwanza inaendelea kuongezeka, na kuongeza kuwa baadhi ya shule za umma zimelazimika kusitisha usajili wa wanafunzi wapya kutokana na ukosefu wa madawati yakutosha.
"Taifa hili limeshuhudia idadi kubwa ya wanafunzi wanaojiunga na shule za umma na shule kadhaa zimepata ugumu wakuwasajili wanafunzi wapya kwa ukosefu wa madawati yakutosha. Kila mtoto ana haki yakupata masomo na yafaa Wizara ya Elimu ipeane pesa zakutosha kwenye shule zote za umma ili kuziwezesha kununua madawati," alisema Ondigi.
Ondigi aidha aliwasihi walimu na wanafunzi kufanya juhudi ili kuimarisha matokeo ya mitihani ya kitaifa kwa kuwa asilimia kubwa ya wazazi wamepoteza imani na mitihani inayo tahiniwa nchini.
"Hali ya elimu nchini imekuwa ikidorora kwa karibu miaka kumi sasa na ningependa kuwahimiza walimu pamoja na wanafunzi kutia juhudi ili kuhakikisha kuwa hali hiyo hairejei tena kwa kuwa tayari asilimia kubwa ya wazazi wamepoteza imani na mitihani inayo tahaniwa nchini,” alisema Ondigi.