Gavana wa kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua, amesema kwamba elimu ndio msingi wa maisha ya kizazi kijacho, na serikali yake imejizatiti kuhakikisha kwamba inasaidia wazazi katika kuelimisha watoto wao.
Akizungumza katika shule ya upili ya Tamunyotta iliyo Kuresoi Kaskazini mnamo Alhamisi, gavana Mbugua alisema hivi karibuni shule hiyo itapata sura mpya kwani serikali yake itafadhili ujenzi wa madarasa na maeneo mengine ya kuimarisha usafi wa wanafunzi.
“Nimeamrisha wahandisi wa serikali ya kaunti yetu ya Nakuru kutembelea shule ya upili ya Tamunyotta na kuangalia jinsi wanaweza wakasaidia katika ujenzi wa madarasa na vyoo,” alisema gavana Mbugua, katika siku yake ya pili ya kutangamana mashinani na wananchi wa Kuresoi Kaskazini.
Serikali ya kaunti ya Nakuru imehamishia majukumu yake yote katika kaunti hiyo ndogo, wadi ya Nyota, ambapo idara tofauti zinapokea mapendekezo, maoni na malalamishi kutoka kwa umma, kwa nia ya kuboresha huduma.
Gavana Mbugua alikuwa pamoja na naibu wake Joseph Rutto kati ya viongozi wengine wa eneo hilo, na makao makuu ya kaunti.