Shule ya msingi ya Spaki na Shule ya Ganjoni ni kati ya Shule za msingi za umma katika Kaunti ya Mombasa zilizoorodhesha wanafunzi bora katika mitihani ya KCPE ya mwaka wa 2015.
Shule ya msingi ya Spaki ilitoa mwanafunzi bora Samuel Munguti Wanza aliyeibuka na alama 422, na shule ya msingi ya Ganjoni ikitoa mwanafunzi bora Swabra Rishaad na alama 415 licha ya wizara ya elimu kutangaza kuwa shule za msingi za umma hazikufanya vyema.
Katika mahojiano na mwahabari huyo mjini Mombasa sku ya Alhamisi, Mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi ya Spaki Nthiga Alfred alisema kuwa zaidi ya wanafunzi wanne katika shule hiyo wamepata zaidi ya alama 400 katika mitihani hiyo.
Nthiga amesema kuwa shule za msingi za umma na zile za kibinafsi hazipaswi kulinganishwa katika matokeo ya mitihani kwani shule za umma husajili wanafunzi wengi kutokana na kuwa shule hizo hutoa elimu ya bure.
"Itakuwa vyema iwapo matokeo ya KCPE haitalinganishwa na shule za kibinafsi kwa sababu shule za umma husajili watoto wengi zaidi kutokana na kuwa shule hizi zetu ni shule za umma na masomo yake ni bure, kwa hivyo sisi nasi pia tumefanya vyema na tunastahili kupongezwa," alisema Nthiga.
Kwa upande wake mwanafunzi wa shule ya msingi ya Spaki Samuel Munguti alisema kwamba kupitia ushirikiano mwema wa walimu pamoja na wazazi na kuzidi kuwa na nidhamu kumemsaidia kufanya vyema katika mitihani hiyo.
"Ninashukuru Mungu pamoja na walimu na wazazi kwa kutusaidia kufanya vyema katika mitihani ya kitaifa ya KCPE, na tunaomba serikali kuhakikisha kuwa shule za msingi za umma zinapewa nafasi zaidi kimasomo," alisema Mungutu, mwanafunzi wa shule ya Spaki aliyeibuka na alama 422.
Wadau mbalimbali wa sekta ya elimu wamepongeza juhudi hizo, huku wakisema kuwa watahakikisha kuwa wanaekeza zaidi katika shule za msingi za umma zinaongoza katika matokeo ya mitihani ya kitaifa ya KCPE.