Mkurugenzi wa sekta ya elimu katika kaunti ya Kisii Richard Chebkawai amesema shule zote za umma katika kaunti hiyo zitakabidhiwa hati miliki ndani ya mwaka mmoja unusu ujao.
Kulingana na Chebkawai shughuli hiyo ya kuhakikisha shule zimepata hati miliki zao imeanza rasmi huku akisema shughuli hiyo inafanywa kufuatia agizo la Rais Uhuru Kenyatta ambaye aliagiza kila shule ya umma kupata hatimiliki.
Akizungumza nasi afisini mwake siku ya Ijumaa, Chebkawai alisema wizara ya elimu nchini inashirikiana na tume inayosimamia ardhi nchini kuhakikisha kila shule imepata hatimiliki hizo.
Katika kaunti ya Kisii, shule za msingi na za upili za umaa ziko zaidi ya 700 ambazo zinatarajiwa kupata hati miliki hizo.
“Tutahakikisha kila shule imekabidhiwa hati miliki maana Rais aliagiza shule zote kupata hati hizo,” alisema Chebkawai.
Kwa majuma mawili yaliyopita mwenyekiti wa Tume ya Ardhi nchini, Mohammed Swazuri alitembelea kaunti ya Kisii na kutoa makataa ya wiki mbili kwa wanyakuzi wa mashamba ya serikali kuondoka kwa hiari lau sivyo waondolewe.
Visa vya unyakuzi wa mashamba katika kaunti hiyo vimekuwa kwa kiwango cha juu zaidi jambo ambalo ni kinyume na sheria.