Mwenyekiti wa chama cha ODM katika eneo bunge la Nakuru magharibi Shem Osiago ametaja siasa kama kizingiti kikuu cha maendeleo katika kaunti.
Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa mwingiliano wa siasa katika serikali za kaunti imesababisha malengo ya ugatuzi kukwama hapa nchini.
Akizungumza hii leo, Jumatatu, mwenyekiti huyo ameunga mkono hatua ya muungano wa Cord ya kuwasilisha sahihi kwa tume huru ya uchaguzi na mipaka ya kupendekeza kufanyika kura ya maamuzi inayolenga kuongeza pesa katika kaunti mbalimbali humu nchini.
Aidha, amesifia hatua hiyo ambayo imetajwa kama kampeni ya okoa Kenya, baada ya wakenya mbalimbali kupeana majina na sahihi zao kwa lengo ambalo amedai itawanusuru wakenya wengi kutokana na umaskini.
Osiago amesema kuwa ikiwa hatua hiyo itafaulu, huduma za kiafya, elimu ya chekechea, kilimo ambazo zimegatuliwa zitaweza kuimarishwa hata zaidi.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo amesema cha msingi ni kuwa pesa zaidi ambazo zinanuiwa kupatikana baada ya kura ya maamuzi baada ya kampeni ya Cord ya 'Okoa Kenya', kuna haja ya kubuniwa kwa afisi ya mwanasheria mkuu katika kila kaunti ambayo itahakikisha uwajibikaji.
Amesisitiza kuwa afisi hiyo itazuia uvujaji wa pesa za kaunti ambazo ni pesa za umma na hata kumsaidia mkaguzi mkuu wa pesa za serikali kuona kuwa ripoti zinaandaliwa na kutolewa kwa wakati na muda ufaao.
Itazingatiwa kuwa hadi kufikia sasa kampeini ya 'Okoa Kenya' iliweza kukusanya zaidi ya kura milioni moja unusu kutoka kaunti zote 47.