Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwenyekiti wa ODM katika eneo bunge la Nakuru Magharibi Shem Osiago amewashutumu vijana wasiojibidiisha kutafuta ajira ilhali wanatumia muda wao mwingi kuzungumza maswala ya siasa na wenzao katika maeneo mbalimbali katika mji wa Nakuru.

Akitoa shutuma hizo, Osiago alitaja vijana hao kama walio na umri chini ya miaka 30 akisema kwamba maswala ya kisiasa ambayo kwa kawaida vijana hao huzungumzia huwa hayawasaidii kujiendeleza maishani na kukimu maisha yao ya kila siku.

Osiago anadai kwamba waume hao pia hutumia muda wao mwingi kwenye baadhi ya hoteli za mji wa Nakuru kuzungumzia maswala ya kisiasa huku wakiwaacha wake zao kutafutia familia zao.

Akizungumza mjini Nakuru , Osiago alitaja jambo hilo kama lisilofaa ikizingatiwa kwamba uchaguzi mkuu ujao ungali mbali huku akidai kwamba baadhi ya wale walio na mtindo huo hawana vitambulisho vya kitaifa na wala hawajajisajili kama wapiga kura.

Badala yake, aliwataka vijana hao kutafuta ajira katika sekta mbalimbali kama vile ile ya jua kali huku pia akikariri kwamba wengine wao wanaweza kutafuta mikopo ya kuweza kuwasaidia kuanzisha biashara mbalimbali.