Share news tips with us here at Hivisasa

Huenda Gavana wa Kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho akapata wakati mgumu katika uchaguzi ujao baada ya kuchipuka wanasiasa wengine ambao wana azma yao ya kuwania ugavana wa kaunti.

Wachanganuzi wa maswala ya kisiasa wamesema kuwa kaunti ya Mombasa inahitaji ushirikiano mwema na ukakamavu wa viongozi na wakazi kwani ikawa mchakato mkali wa kisiasa utashuhudiwa katika kaunti hiyo, basi utakuwa na upinzani mkubwa.

Wachanganuzi hao wa maswala ya kisiasa wakiongozwa na Wakili Jahnson Muchiri wamesema kuwa kila mmoja anatarajiwa kuonyesha ubabe wake wa kisiasa, lakini kwa kutumia njia ya amani na uelewano na jamii basi uchaguzi huo utakuwa huru na wa haki.

Muchiri amesema kuwa ni vyema wanasiasa hao kufanya siasa za amani na kujitenga na siasa za uchuki na uchochezi ili kuzuia kuwagawanya wakenya wanaowaunga mkono katika mchakato huo wa kisiasa.

"Tunajua sasa siasa za Mombasa zitakuwa na ushindani mkali, lakini kitu tunaomba ni kuwa wafanye siasa zao kwa amani na wajitenge na matamshi ya chuki na uchochezi ili kuzuia mafarakano,” alisema Muchiri.

“Ukweli ni kwamba siasa za Mombasa zitakuwa na wakati mgumu wa viongozi hao kuwashawishi wakazi," aliongeza Muchiri kwenye mahojiana ya kipekee na mwanahabari huyu siku ya Jumatatu.

Waliotangaza kuwania ugavana wa kaunti ya Mombasa katika uchaguzi mkuu ujao ni Gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho, Seneta wa kaunti hiyo Hassan Omar Sarai, Mbunge wa Nyali Hezron Awiti Bollo, Mfanyibiashara wa Mombasa Suleiman Shahbal na Naibu Gavana wa kaunti ya Mombasa Bi Hazel Katana.