Mbunge wa Kitutu Masaba Timothy Bosire ametetea rekodi ya utendakazi wake kwenye wadi ya Gesima, huku akiwashtumu wapinzani wake wa kisiasa kwa upinzani unaomkabili kutoka kwa baadhi ya wakazi wa wadi hiyo.
Bosire aliongeza kwa kusema kuwa pesa za hazina ya maendeleo ya maeneo bunge lake zimekuwa zikitumika kukarabati shule nyingi katika wadi hiyo, huku akiongezea kusema kuwa ukarabati wa barabara ya Metamaywa- Kebirigo ni moja wapo ya miradi anayo ifadhili.
"Ninaongozwa na sheria kwenye utendakazi wangu na ninapotumia pesa za wananchi kwenye miradi lazima ni hakikishe kwamba pesa hizo zinatumika vizuri bila uvujaji wa aina yeyote kwa mfano ujenzi wa maabara ya shule ya upili ya Riakworo na Karantini umekamilika kupitia kwa ufadhili wa CDF, na ni kupitia kushinikisha kwangu serikali ndipo barabara ya metamaywa ikakarabatiwa," alisema Bosire.
Mbunge huyo aidha aliwalaumu vijana wa eneo hilo kwa kutojiunga katika makundi ili angau aweze kuwasaidia akiongezea kusema kuwa nia yake ni kufanya kazi katika wadi zote sita za eneo hilo bila ubaguzi.
"Shida yenu vijana ni kuongea tu bila kuchukua hatua yeyote ile na sina hakika iwapo kuna kikundi cha vijana ambacho kimewahi kuja kwangu nikakataa kuwasaidia, na huenda ikawa kama vikundi hivyo vipo basi havijasajiliwa," alisema Bosire.
Mwekahazina huyo wa kitaifa wa chama cha ODM alikuwa akihutubia vijana katika kijiji cha Ritibo siku ya Jumatano baada ya vijana hao kumwandikia barua kulalamikia kutenga kwake eneo hilo kimaendeleo.