Wakaazi wa kaunti ya Nakuru waliungana na dunia nzima kuadhimisha siku ya ukimwi duniani jumanne, kauli mbiu ikiwa kutokomeza virusi hivyo au Getting to Zero.
Maadhimisho hayo yalifanyika katika bustani ya nyayo mjini Nakuru huku baadhi ya waliohutubia waliofika kwenye mkutano huo wakiwahimiza wakenya wapimwe ili wajue hali zao za kiafya.
Walihimizwa pia kuungana ili kutokomeza ukimwi.
Afisa mkuu wa afya katika kaunti ya Nakuru daktari Samwel Mwaura alikariri kwamba wakati umewadia wa kuwashirikisha vijana katika harakati za kukabiliana na kutokomeza virusi vya ukimwi hapa nchini.
“Pamoja tuangamize ukimwi. Tunapoadhimisha siku hii , tukumbuke kuwa ni mwaka wa thelathini na moja tangu kulipobainika kuna maambukizi ya virusi vya ukimwi hapa nchini, tunahitaji sasa kufikiria jinsi tutakavyowashirikisha vijana katika kukabiliana na virusi hivi. Tunahitaji pia kujua wasichana wetu ni wa aina gani. Tunapozungumzia kuhusu wasichana wetu, tunaangazia kuhusu wasichana wanaopata uja uzito mapema wakiwa wachanga. Tunapoangazia siku hii, tunafaa kufikiria kuhusiana na maambukizi ya virusi vya ukimwi miongoni mwa vijana,’ alisema daktari Mwaura.
Naye naibu kamishna mkuu wa kaunti ya Nakuru Catherine Njoroge alikariri kuwa kaunti ya Nakuru na serikali kuu zinajibidiisha kutokomeza ukimwi nchini.
“Serikali kuu na ile ya kaunti zimejitolea kuhakikisha kwamba hakuna virusi vya ukimwi hapa nchini. Hivyo basi, tumeanza kuwahusisha wadau katika sekta mbalimbali katika majadiliano jinsi ya kuafikia hili,” alisema bi Njoroge.
Aliangazia pia swala la utokomezaji wa maambukizi ya virusi vya ukimwi kutoka kwa mama hadi kwa mtoto akisema kampeni inayoendelezwa na mama wa taifa Margaret Kenyatta imechangia pakubwa katika kuafikia hilo.
“Kampeni ya Beyond Zero inayoendelezwa na mama wa taifa ni hatua kubwa katika kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa katika vituo vyote vya kimatibabu,” alisema naibu huyo wa kamishna.