Mbunge wa eneo bunge la Jomvu Badi Twalib amesema kuwa hana nia ama mipango yoyote ya kuwania kiti cha useneta wala ugavana katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
Akizungumza na mwanandishi huyu katika ofisi yake kwenye eneo la Jomvu siku ya Jumanne Twalib alisema kuwa hayuko tayari kwa sasa kuwania nyadfha hiyo na badala yake anataka kuwaongoza wakaazi wa Jomvu na kutimiza ahadi zake.
Twalib alisema kuwa bado hajamaliza malengo aliyo nayo na miradi ambayo wanajomvu wanastahili kupata kufikia sasa, na kuwa anatarajia kuwania kiti cha ubunge katika eneo lake ifikapo mwaka wa 2017.
Aidha, aliongeza kuwa ana imani kubwa na wakaazi wa Jomvu, kwasababu miradi ambayo ameianza bado haijakamilika na anahitaji muda zaidi.
Aidha, mbunge huyo alisema kuwa yuko tayari kushirikiana na wakaazi wa Jomvu na ofisi zake ziko kwa wazi kwaajili ya kutenda kazi ya mwananchi ambaye alimchagua.
Kiongozi huyo alisema kuwa nia na madhumuni yake ya kuwania tena kiti hicho ni kuwa anataka kuzidi kusaidia eneo hilo na kutatua changamoto ambayo wamekuwa wakikumbana nayo ya unyakuzi wa mashamba.