Mwakilishi wa wadi ya Bahati katika bunge la kaunti ya Nakuru, amepuuzilia mbali madai aliyosema yanayoenezwa katika eneo bunge la Bahati kwamba yeye pamoja na baadhi ya wawakilishi wa wadi bungeni la kaunti hiyo, wanazuilia ukarabati wa barabara zilizotengewa serikali kuu.
Akizungumza Jumapili kwenye hafla ya kuchangisha fedha kumsaidia kasisi aliyechomekewa na makaazi katika soko la Wanyororo ‘B’ wadi ya Bahati, Peter Nderitu Mwangi maarufu kama Birishiba, alisema kuwa kuna uvumi unaonenezwa kwamba anazuilia barabara zikarabatiwe.
"Nani kati yenu ameniskia nikihutubia watu kwamba sitaki barabara fulani ikarabatiwe, ama kwenye chombo chochote cha habari? Wakati wa siasa haujafika na hizo ni siasa tupu, mtu ajitafutie kura za 2017 kwa kazi anayofanya, si kwa kuharibu sifa na kazi yangu,” alisema Nderitu.
Hata hivyo alipasua mbarika zaidi kwa kusema kwamba baadhi ya wapinzani wake wa kisiasa wameanza kueneza propaganda zingine kuwa anapania kuwania kiti cha ubunge katika eneo bunge la Bahati.
“Mimi sina nia ya kupigania ubunge 2017. Kwani nina nguvu na mamlaka kiasi gani hata kuweka wengine kiwewe ili watafute kura kwa kusema ninapinga ukarabati wa barabara?” alihoji Nderitu.
Hapo kabla alikuwa katika kanisa la Full Gospel Landimawe, ambapo aliwataka wakristu kudhihirisha uongozi mwema na kuwa mfano kwa jamii.
Huku uchaguzi mkuu ukiwa umebakisha takriban miezi 18, zaidi ya watu 20 wamejitokeza kuwania kiti hicho cha mwakilishi wa wadi ya Bahati, bungeni la kaunti ya Nakuru.