Rais Uhuru Kenyatta amesema kuwa serikali yake itahakikisha kuwa soko la Kongowea, ambalo ni kubwa zaidi Afrika Mashariki litaboreshwa na kufanyiwa usafi ili kufikia viwango vya mataifa.
Akiongea siku Jumanne katika soko hilo la Kongowea, Rais Uhuru aliwataka washika dau wote kuunga mkono mikakati ya serikali yake ili kuinua uchumi wa nchi hii, huku akisema kuwa soko hilo ni miongoni mwa masoko machache nchini ambayo yanawapa raia hasa vijana nafasi nyingi za kazi.
Aidha alisema kuwa lengo la serikali yake ni kuweka miundomsingo imara ili kupanua nafasi zaidi za watu kufanyia shughuli zao za kibiashara.
Rais pia aliwahakikishia wawekezaji kuwa huru kuwekeza miradi yao katika nchi ya Kenya ili kuona kuwa kazi zinapatikana na uchumi wa nchi unakua.
Wafanyabiashara wa soko hilo aidha wameitaka serikali kuu kufanya ushirikiano na serikali ya Kaunti ya Mombasa ili kutekeleza matakwa yao, na wakatoa wito kwa serikali zote mbili ziangalie ushuru ambao wanadai uko juu na mara kwa mara inakuwa vigumu kwa baadhi yao kufanikisha malengo yao ya kulea familia kwa ada hizo kuwa juu.
Walitia dosari serikali ya Kaunti kwa kukosa kukarabati miundomsingi ya soko hilo licha ya wao kuwatoza ushuru kila siku.