Hatua ya mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Mombasa Mishi Mboko kuandamana na kumtaka Seneta wa Nairobi Mike Sonko kuwaomba msamaha wakazi wa Mombasa na gavana Ali Hassan huenda ikamgharimu kisiasa.

Share news tips with us here at Hivisasa

Hii ni kufuatia tamko la Sonko kuwa atafanya lolote chini ya uwezo wake ikiwemo kupiga kambi mkoani Pwani ili kuhakikisha kuwa Mboko hashindi kiti chochote cha kisiasa katika uchaguzi ujao.

Sonko anadai kuwa hakufanya kosa lolote siku ya Jumamosi iliyopita katika hafla ya kuwapa hati miliki maskwota 5,000 wanaoishi katika shamba la Waitiki, alipowataja viongozi wa upinzani kuwa wasaliti wa serikali wasiomheshimu Rais Kenyatta hivyo hataomba msamaha wowote.

''Nilisema ukweli, Gavana Joho na wenzake katika upinzani hawana heshima kwa Rais. Hakuna kosa lolote hapo na sitaomba msamaha,'' alisema Sonko.

Sonko aidha amemtaka Mboko kutolihusisha jina la babake na masuala ya ardhi wala siasa.

Seneta huyo alikuwa akizungumza siku ya Jumanne alipozuru afisi za CDF zilizoko katika eneo bunge la Likoni ambapo alitoa shilingi milioni mbili ili kuiendeleza miradi ya wanawake katika eneo bunge hilo.

Kauli yake iliungwa mkono na mbunge wa Likoni Masoud Mwahima, aliyeapa kwa mara nyingine tena kuwa atakitetea kiti chake kwa tiketi ya chama kipya cha JAP katika uchaguzi ujao.

Siku ya Jumapili iliyopita, Mishi Mboko aliandamana na zaidi ya wanawake 500 nyumbani kwake na kumkashifu Sonko kwa madai ya kuwakosea heshima viongozi wa mkoa wa Pwani kwa kuwataja wanafiki na wasaliti wa serikali.