Share news tips with us here at Hivisasa

Uhasama wa kisiasa baina ya Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho na Seneta wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko huenda ukapamba moto iwapo seneta huyo atauitikia wito wa kuwania kiti cha ugavana wa Mombasa katika uchaguzi ujao.

Sonko ambaye alizaliwa mjini Mombasa kabla kuihamia Nairobi baada ya kuyamaliza masomo ya shule ya upili, amekuwa akiandaa mikutano na makundi ya wazee na wanawake mjini humo katika ziara yake na Rais Uhuru Kenyatta.

Wikendi iliyopita, seneta huyo alikutana na viongozi wa jamii ya Mijikendi ambapo duru zinaarifu kuwa viongozi hao, walimtaka awanie kiti cha ugavana wa Mombasa katika uchaguzi wa 2017.

Akizungumza mjini Momabasa siku ya Jumatano, msemaji wa mrengo wa Jubilee katika Kaunti ya Mombasa, Matano Chengo, alimtaja Sonko kama mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa, ambaye ana uwezo wa kuzoa ushindi katika eneo lolote nchini.

“Sonko anapendwa na wengi. Kila anapokwenda wananchi wanamshangalia kwa hivyo akisimama Mombasa ushindi ataupata,” alisema Chengo.

Kwa upande wake, seneta huyo, ambaye amekuwa akiandamana na Rais Uhuru Kenyatta kaitika ziara zake katika eneo la Pwani kwa zaidi ya majuma mawili sasa, alisema atalifikiria suala kabla kuchukua hatua.

Sonko alisema kuwa kwa sasa yuko Pwani kwa minajili ya kutekeleza maendeleo.

Haya yanajiri majuma mawili tu tangu Sonko na Gavana wa Mombasa Hassan Joho, kujibizana mbele ya Rais Uhuru Kenyatta katika hafla ya utoaji hati miliki kwa wakaazi wa Shamba la Watiki.