Share news tips with us here at Hivisasa

Katibu Mkuu wa chama cha walimu, Knut, Wilson Sossion ametakiwa kukoma kujihusisha na maswala ya waalimu waliostaafu.

Onyo hilo limetolewa na zaidi ya waalimu elfu 52 walio chini ya kundi la waalimu waliostaafu mwaka wa 1997 ambao mahakama ya Nakuru iliagiza walipwe shilingi bilioni 42.3 .

Wakiongozwa na mwenyekiti wao David Mwenja na katibu wa chama hicho Gidraph Kimatta waliokuwa wakiwahutubia wanahabari mjini Nakuru siku ya Alhamisi, waalimu hao wamesisitiza kwamba matamshi ya Sossion ya Jumatano yaliyokuwa kwenye gazeti moja la humu nchini ya kuitaka serikali kuwalipa waalimu hao waliostaafu fedha hizo katika muda wa siku 30 hayafai kwani hao si wanachama wa Knut.

Walimu hao wastaafu, kupitia kwa katibu wa chama chao badala yake wamemtaka Sossion kujibidiisha kuwapigania waalimu na maswala ya walimu waliomchagua badala ya kutoa makataa kwa serikali kuwapa waaalimu wastaafu pesa zao.

Mwenja aidha amedokeza kuwa waliwasilisha kesi mahakamani dhidi ya tume ya kuwaajiri waalimu TSC na mkurugenzi wa fedha za wastafu kama kundi huru la waliostaafu na kutokana na hilo, hawahitaji usaidizi wa chama cha Knut kushinikiza serikali kuwalipa.

Aidha, wamemtaka Sossion kutotumia kundi hilo kujipatia umaarufu iwapo nia yake ni kutaka kuwania kiti chochote cha kisiasa, huku akiwahimiza wanachama wa kundi hilo la wastaafu kuwa wenye subira kwa kuwa wakili wao anafuatilia kwa makini swala la kuhakikisha wanapokea fedha zao.

Mahakama iliagiza wastaafu hao walipwe fedha hizo baada ya kesi hiyo kuendelea kwa muda wa miaka 10 mahakamani.