Spika wa bunge la kaunti ya Nyamira Joash Nyamoko amejitokeza kuzitaka serikali za kaunti na ile ya kitaifa kupitisha miswada bungeni ili kuhakikisha kuwa matumizi ya pesa za umma na maafisa wa serikali yanathibitiwa. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akihutubia wanahabari mjini Nyamira siku ya Jumatatu, Nyamoko alisema kuwa ili agizo la Rais Kenyatta la kupunguza matumizi ya pesa serikalini litekelezwe, sharti kuwepo sheria ya kuthibiti matumizi ya pesa serikalini. 

"Kwa kweli ninaunga mkono hatua ya rais Kenyatta kutaka kupunguza matumizi ya pesa serikalini ila hilo linaweza tu kuafikiwa iwapo mabunge ya kaunti na lile ya kitaifa yatapitisha sheria za kuhakikisha kuwa agizo la Rais linatekelezwa," alisema Nyamoko. 

Nyamoko aidha alisema huenda ikawia vigumu spika wa mabunge ya kaunti na magavana kutekeleza agizo hilo huku ikizingatiwa kuwa wawakilishi wadi ndio walio na uwezo wa kuchunguza matumizi ya fedha kwenye serikali za kaunti. 

"Ninaunga mkono suala hili la kupunguza matumizi ya pesa serikalini, ila ninahofia kuwa huenda wawakilishi wadi wakahujumu utendakazi wetu maspika pamoja na magavana kwa kuwa wao ndio walio na uwezo wa kuasisi jinsi pesa zinavyotumika katika kaunti," aliongezea Nyamoko.