Spika wa bunge la kaunti ya Nyamira Joasha Nyamoko amejitokeza kuwahimiza wawakilishi wodi katika bunge hilo kuzingatia umoja na uwazi wakati wa kujadili miswada mhimu ya maendeleo.
Akihutubia bunge hilo wakati wa ufunguzi rasmi wa bunge hilo lililokuwa kwenye likizo ya miezi miwili, Nyamoko aliwahimiza wawakilishi wadi kuunga au kupinga miswada inayowasilishwa bungeni kwa kuzingatia uwazi bila ya kuzingatia inapoegemea milengo ya kisiasa wanayoiwakilisha bungeni.
"Jukumu la bunge hili ni kuidhinisha sheria muhimu za kuimarisha maendeleo hapa Nyamira na pia kuhakikisha kuwa tunahakikisha mgao wa pesa za maendeleo kwenye kaunti unatumika vizuri," alisema Nyamoko.
"Ni jukumu letu kuhakikisha kuwa tunaiunga au kupinga miswada kwa kuzingatia jinsi inavyoathiri maisha ya wananchi na sio tu kwa kuzingatia inapoegemea milengo yetu ya Kisiasa," aliongeza Nyamoko.
Nyamoko aidha aliwahimiza wawakilishi wadi kufanya vikao muhimu ili kuafikia mwafaka kuhusiana na miswada mhimu kama njia mojawapo ya kupunguza wakati wa kujadili miswada hiyo bungeni.
"Ningependa kuhimiza milengo yote ya kisiasa kuhakikisha kuwa wanafanya vikao na kujadili miswada ya bunge hili badala ya kungoja hadi miswada hiyo ifikishwe bungeni ili kuonyesha ubabe wa kisiasa kwa maana maendeleo ndio muhimu zaidi," aliongeza Nyamoko.