Wanachama wa kamati mbalimbali kwenye bunge la kaunti ya Nyamira wameonywa vikali dhidi ya kuwasilisha ripoti hafifu kwenye bunge la kaunti hiyo.
Akihutubu kwenye kikao na wawakilishi wa wadi Jumatano jioni, spika wa bunge hilo Joash Nyamoko alisema kuwa kwa muda sasa amekuwa akishangazwa na mazoea ya baadhi ya kamati kuwasilisha ripoti zisizo na uzito mbele ya bunge hilo, hali inayosababisha bunge hilo kuwa na ugumu wa kuafikia malengo yake.
Spika huyo aliwasihi wenyekiti wa kamati mbalimbali kuzingatia majukumu yao kama njia mojawapo ya kuipa hadhi bunge la kaunti hiyo linalostahili kwa maswala yake ya uangalizi, uwakilishi na utunzi sheria.
"Kama spika wa bunge la kaunti, mimi hushangazwa na kuwasilishwa kwa ripoti hafifu na zisizo tamatika mbele ya bunge hili ili kujadiliwa, na inafaa ripoti ambazo zinawasilishwa hapa ziwe na uzito na zilizotamatika kwa minajili ya kuepukana na lalama za wananchi," alisema Nyamoko.
Nyamoko aidha alionya kuwa huenda akalazimika kuchukua hatua kali ili kuziadhibu kamati husika, huku akiongeza kusema kuwa kamati hizo hazistahili kuhoji idara husika kabla ya kuandika ripoti.
"Kama spika wenu niko tayari kuchukua hatua kuhakikisha kuwa kazi inafanywa kwa maana pesa za umma sharti zitumike vizuri katika kuzichunguza idara mbalimbali kama njia mojawapo ya kuwa na uwazi na kutokuwa na mapendeleo," alionya Nyamoko.
Spika huyo aliongeza kwa kuwahimiza wawakilishi wadi kutokosa kuhudhuria vikao vyote vya bunge, labda tu wawe na ruhusa rasmi kutoka afisini mwake.