Baraza la maimamu nchini SUPKEM limewapongeza wanawake wakiislamu kwa juhudi zao za kuwatetea na kusimama na wakristo katika shambulizi la kigaidi na wanamgambo wa Alshabaab.
Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya jumanne, katibu mtendaji wa Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini CIPK, Sheikh Mohammed Khalifa, alitaja hatua ya wanake hao kama ya kishujaa inayofa kuigwa na wengi.
Khalifa vile vile alisema kitendo cha wanawake hao ni dhihirisho tosha kuwa dini ya Kiislamu haiungi mkono ugaidi wala haijihusishi na tendo lolote la kigaidi.
''Wanawake hao wanathibitisha kuwa Wakenya hawako tayari kugawanywa katika msingi wa kidini na hivyo kila mmoja anafaa kusaidia mwenzake bila kujali kabila lake wala dini yake,” alisema kiongozi huyo.
Wanawake wakiislamu waliwalinda wenzao wakristo kwa kukataa kugawanywa kwa makundi baada ya basi walimokuwa wakisafiria kutekekwa nyara na wanamgambo wa Alshabaab siku ya Jumatatu asubuhi.
Inadaiwa basi hilo lilokuwa likielekea eneo la Mandera Kaskazini kutoka Nairobi lilitekwa nyara na wapiganaji wa Alshabaab na hapo ndipo abiria waliamuriwa kujigawanya katika makundi.
Hata hivyo, kulingana na walioshuhudia tukio hilo, wanawake wa wakiislamu walikaidi agizo hilo huku wakivua hijab na kuwastiri wanawake wakristo ilikuwaokoa wasiuawe.
Mwezi Novemba mwaka wa 2014 wapiganaji wa Alshabaab waliteka basi moja na kuwaua abiria 28 ambao hawakuwa Waislamu.