Mwenyekiti wa tume ya kitaifa ya ardhi Muhammed Swazuri ametoa onyo kwa wananchi walio na mtindo wa kuuza vipande vya ardhi kiholela.
Swazuri alisema kuwa hatua hii itasaidia pakubwa kupungua kwa maskwota mkoa wa Pwani pindi tu wananchi watakoma kuuza ardhi zao kwa mabwenyenye kisha kudai kuwa hawana mashamba.
Swazuri alisema haya siku ya Ijumaa kuwa watakaopatikana watachukuliwa hatua za kisheria, hasa wale wanaojihusisha na uuzaji ardhi ambazo si zao.
Aidha, aliongeza kuwa serikali inajizatiti kukabiliana na mizozo ya mashamba nchini na kuhakikisha kuwa kila raia anamiliki kipande cha ardhi kihalali.
Swazuri aliyasema haya baada ya kukubaliana na wanachama wa bodi inayomiliki shamba la Dhadhini na Hussein Dairy kujadiliana kuhusu sehemu za vipande vya ardhi vitakazogawanywa kwa wananchi.
Aidha, alisisitiza kuwa ugavi huo wa ardhi hizo utazingatia asili ya waliokuwepo tokea zamani ili kuepuka uvamizi na vurugu za mara kwa mara zinazosababishwa na wananchi .
Miongoni mwa mashamba yatakayogawanywa kwa wananchi ni Dhadhini yenye ekari 4,320 kwa Muithopia, Zumzum na Hussein Dairy yenye ekari 420.