Mbunge wa Kitutu Masaba ameshtumiwa Timothy Bosire vikali kwa ‘kuwatenga’ baadhi ya wawakilishi wadi kutoka eneo bunge lake katika agenda yake ya kustawisha eneo hilo kimaendeleo.
Akihutubu katika eneo lake la uwakilishi wadi, mwakilishi wa wadi ya Rigoma Benson Sironga alisema kuwa Bosire amekuwa na mazoea ya kuwatenga baadhi ya viongozi waliochaguliwa, huku akisema kuwa mbunge huyo amekuwa akitekeleza miradi ya maendeleo bila kuwashauri viongozi wengine.
“Bosire hutekeleza miradi ya maendeleo bila ya kuhusisha viongozi wa kisiasa kutoka eneo hili, na kwa kweli maeneo mengine yamekuwa yakitengwa kwa kutopokea pesa za kufadhili miradi mbalimbali, na uongozi wa aina hiyo umepitwa na wakati, inafaa kila kiongozi ashauriwe kabla ya miradi yeyote kutekelezwa,” alihoji Sironga.
Mwakilishi huyo wa wadi aidha alisema kuwa mbunge huyo amekuwa na mazoea ya kupendelea wadi za Kemera, Manga na Magombo, huku akitenga Rigoma, Gachuba na Gesima kwenye agenda yake ya maendeleo.
“Huu ni wakati ambapo mbunge wa eneo hili anastahili kufanya kazi hasa kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye wadi zote kwa maana wadi za Gesima, Rigoma na Gachuba zimekuwa zikitengwa kwa muda sasa,” alisema Sironga.