Tume ya kutetea haki za binadamu nchini sasa inasema serikali ndiyo inafaa kulaumiwa kwa huduma mbovu inayotolewa na halmahsauri ya bandari badala ya viongozi wake.
Tume hiyo, kupitia mkurugenzi mtendaji Julius Ogogoh inadai serikali haijakuwa ikitekeleza wajibu wake ipasavyo, na badala yake kumtia lawamani mkurugenzi anayesimamia huduma za feri Musa Hassan kufuatia malalamishi ya mara kwa mara inayotolewa na wasafiri wanotegemia huduma za feri.
Kulingana na Ogogoh, serikali imekuwa ikitoa kiasi kidogo cha pesa kwa usimamizi wa feri, na hivyo kufanya mazingira ya kazi kuwa magumu kwa viongozi wake.
"Katika bajeti ya mwaka 2015/16 usimamizi wa feri ulipendekeza shilingi milioni 917, lakini serikali ikatenga shilingi milioni 336 pekee ambapo mpaka sasa usimamizi huo umepokea shilingi milioni 168 pekee,'' alisema Ogogoh.
Halmashauri ya bandari kwa huduma za feri imekuwa chini ya shinikizo katika siku za hivi majuzi kutokana na lalama za mara kwa mara kuhusu utendakazi mbovu unaoshuhudiwa katika kivukio cha feri cha Likoni.
Hali hii imepelekea baadhi ya viongozi, akiwemo kamishna wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa na Naibu Gavana Hazel Katana kutaka mkurugenzi anayesimamia huduma za feri atimuliwe kwa madai ya kuzembea kazini.