Share news tips with us here at Hivisasa

Wakaazi wa Mombasa hawana mazoea ya kutembelea mashirika ya kutetea haki za kibinadamu katika eneo hilo na kuwasilisha malalamishi ya dhulma wanazopitia.

Kauli hii ni kwa mujibu wa tume ya kutetea haki ya Ombudsman tawi la Pwani, linalodai kwamba wakaazi wengi wa Mombasa na Pwani kwa jumla hawana ufahamu kuhusu mashirika ya kutetea haki.

Tume hiyo ambayo hushughulikia zaidi dhulma kutoka kwa makampuni pamoja na idara mbalimbali za kiserikali dhidi ya wananchi imesema kuwa kutokana na hali hiyo, wakaazi wengi huishia kuteseka na kupitia dhulma mbalimbali kwa kukosa kuelewa sehemu maalum za kuwasilisha lalama zao.

Akiongea na mwandishi huyu siku ya Jumanne afisini mwake, wakili wa tume hiyo Bi Mumtaz Khan alisisitiza kuwa wananchi wanafaa kutembelea vituo vya sheria ili kujua haki zao za kimsingi.

“Tulifanya utafiti na kugundua kuwa wananchi wengi hupitia dhulma kutoka katika ofisi mbalimbali za umma lakini wanaogopa kuripoti huku hata wengine wakikosa ufahamu kuhusu umuhimu wa kuwasilisha visa hivyo,” alisema Khan.

Khan aliongeza kuwa wananchi wengi wamekuwa wakipitia dhulma za aina mbalimbali kutoka kwa idara ya polisi huku wengine wakipitia vitisho kila wanapowasilisha kesi katika vituo hivyo.

“Idadi kubwa ya watu wanaotembelea afisi yetu huwa wana malalamishi kwamba wamewasilisha kesi katika vituo vya polisi lakini hakuna hatua inayochukuliwa, na tunashukuru tumekuwa tukifuatilia maswala hayo hadi pale wanapopata haki,” aliongeza wakili huyo.

Hata hivyo, tume hiyo imewasihi Wapwani kuelewa kuwa kila Mkenya ana haki, na kuwataka wananchi kuondoa uoga kila wanapopitia dhulma kutoka kwa mashirika yanayoonekana kuwa na ushawishi mkubwa.

Tume hiyo ya Ombudsman ilizinduliwa rasmi humu nchini mwaka wa 2011 chini ya kifungu cha 59 cha katiba mpya kusaidia Wakenya kupata haki dhidi ya dhulma zinazotokana na uongozi mbaya nchini.

Tangu kuzinduliwa kwa tawi jipya Mjini Mombasa kwa niaba ya ukanda mzima wa Pwani mwaka wa 2015, tume hiyo imesaidia kusuluhisha takriban ripoti 10 ambapo walalamishi walifanikiwa kupata haki.