Share news tips with us here at Hivisasa

Idara ya polisi eneo la Pwani imedai kupokea ripoti za kijasusi kuwa kundi lililoharamishwa la Mombasa Republican Council linapanga njama ya kutekeleza mashambulizi wakati wa uchaguzi mkuu ujao.

Maafisa wakuu wa polisi kaunti ya Mombasa, Kilifi, Tana River na Kwale wamedai kupokea ripoti hizo za kijasusi na wakawasilisha katika makao makuu ya idara ya polisi mjini Mombasa, huku maafisa wa polisi na wale wa kupambana na` wahalifu wakituma mashinani.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne, Kamanda mkuu wa polisi eneo la Pwani Francis Wanjohi alisema kuwa kuna baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaowafadhili wafuasi wa kundi hilo la MRC ili kuzua vurugu na kusababisha taharuki katika eneo hili.

"Serikali iko macho kuhakikisha kuwa hakuna mtu yeyote anatatiza usalama wa wananchi na uchaguzi mkuu ujao katika eneo la Pwani na ile kundi la MRC afadhili lijisalimishe na mapema kwa sababu serikali itawakabili kikamilifu," alisema Wanjohi.

Amewataka maafisa wa polisi kuwa waangalifu wanapokabiliana na kundi hilo huku akiwahakikishia wakazi wa eneo la Pwani kuwa usalama umerimashwa na lazima kundi hilo kukabiliwa kikamilifu.

Kundi la MRC linadai kutetea maslahi ya wapwani kutokana na kukithiri kwa dhulma za kihistoria, undamizaji na kupigania ardhi ya Pwani.