Wafanyabiashara katika jiji la Mombasa ambao wana asili ya Kaunti ya Lamu wamewataka wakazi katika kaunti hiyo kutumia nafasi yao kwenye sherehe za kitamaduni za kila mwaka kuungana na kukumbatia utangamano miongoni mwa jamii mbali mbali.
Wakiongozwa na Said Rahemtulah Amir siku ya Jumatano, wanabiashara hao walisema kuwa hafla hiyo ambayo hufanywa kila mwaka azimio lake huwa ni kuwakutanisha watu kutoka matabaka tofauti na ngazi mbalimbali za viwango za kijamii ili kuwaunganisha na kubadilishana mawazo.
Amiri aidha aliwasia kwa vijana kumakinika kila mara sherehe hizo zinafanyika ili kufaidi masuala mbalimbali ya mila na tamaduni, na kuhakikisha kuwa wao kama vijana wanafanya juhudi za kuendeleza utaratibu ambao unafuatwa kwenye ufanisi wa tamaduni hizo za wakazi.
“Dhamira yetu kila tunapofumana na kukutana kwenye sherehe za mila na tamaduni ni kuhakikisha kuwa asili yetu ya mila haipotei, na sharti tuwahusishe watu wa matabaka yote ili sisi tukija kuondoka kuwe mna wengine wa kuchukua usukani na kutanua na kuendeleza tamaduni zetu,” alihoji Amir.
Amir na wenzake waliongea na mwanahabari huyu wakati walikuwa wanaondoka kuenda kushiriki sherehe hizo zinazoandaliwa hii leo, Alhamisi.