Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Idara ya walemavu katika Kaunti ya Mombasa imewataka walemavu kuchukua nafasi ya kutolipa ushuru kufanya biashara na shughuli nyingine za kuwapa riziki ili kuimarisha hali yao ya kiuchumi.

Hii ni kufuatia serikali kuu na serikali za kaunti kuweka sheria za kutowatoza ushuru watu walio na ulemavu.

Kulingana na idara hiyo ya walemavu ambayo iko chini ya Wizara ya Michezo, Jinsia na Masuala ya Vijana, ni bora iwapo watu walio na changomoto za ulemavu wa aina yoyote ile kuanza kuboresha maisha yao kwa kutumia pesa za akiba iliyotengwa kuwainua kimaisha.

Kwa mujibu wa naibu wa mkurugenzi wa watu walio na ulemavu katika Kaunti ya Mombasa, Elvinah Muzungu, serikali za kaunti zimefanya hisani kwa kutowatoza walemavu ushuru wanapofanya shughuli zinazowapa riziki ya kila siku.

“Walemavu wengi hasa katika mitaa ya Mombasa hapo mbeleni walikuwa wakitumia kisingizio kuwa hawana uwezo wa kifedha lakini sasa kwa vile nafasi yao imetambuliwa, sharti wawe tayari kuimarisha hali yao ya maisha,” alisema Muzungu.

Aliongeza, “Serikali ya Kaunti iliweka sera ya kutowatoza walemavu ushuru, hivyo wanafaa kuchukua nafasi hiyo kujifaidi kwa kufanya biashara.”